22nd June 2018 23:58:52

UDAHILI KWA MAFUNZO YA UALIMU NGAZI YA ASTASHAHADA NA STASHAHADA KWA VYUO VYA SERIKALI NA VISIVYO VYA SERIKALI KWA MWAKA WA MASOMO 2018/19

 

UDAHILI KWA MAFUNZO YA UALIMU NGAZI YA ASTASHAHADA NA STASHAHADA KWA VYUO VYA SERIKALI NA VISIVYO VYA SERIKALI KWA MWAKA WA MASOMO 2018/19

Baraza la Taifa la Elimu ya Ufundi (NACTE) linapenda kuwafahamisha wahitimu wa kidato cha nne na sita na umma kwa ujumla kuwa udahili kwa Mafunzo ya Ualimu ngazi ya Astashahada na Stashahada kwa mwaka wa masomo 2018/19 umefunguliwa rasmi kuanzia tarehe 22 Juni 2018 hadi tarehe 8 Septemba 2018 na Masomo yanatarajia kuanza tarehe 04 Octoba, 2018 kama ilivyoelekezwa na Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia.

Aidha, Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia imeelekeza kwamba waombaji wa mafunzo haya ni wale wenye ufaulu wa Daraja la Kwanza hadi la Tatu katika mtihani wa kuhitimu kidato cha NNE (kwa waombaji wa Astashahada (miaka miwili) na kidato cha SITA kwa stashahada (miaka miwili). Aidha, kwa waombaji wa Stashahada (miaka mitatu) wawe na ufaulu wa kidato cha Nne katika masomo ya Sayansi na Hisabati kwa kiwango cha alama ‘C’ katika masomo mawili ya kufundisha.

Baraza linataarifu kuwa sifa za kujiunga na kozi mbalimbali za Ualimu katika Vyuo vya Ualimu vya Serikali na visivyo vya Serikali ni kama zilivyoanishwa kwenye Kitabu cha Mwongozo wa Udahili (Admission Guidebook) kilichopo kwenye tovuti ya Baraza.

Kwa waombaji wa programu za Ualimu katika Vyuo vya Serikali watatakiwa ama kuomba moja kwa moja vyuoni ambako vyuo vitawasajili kupitia ‘Instititutional Panel’ ya chuo husika au wanaweza kuomba kupitia tovuti ya Baraza la Taifa la Elimu ya Ufundi (NACTE) (www.nacte.go.tz) kwa kubofya kwenye ‘Apply online (SAVS)’ kisha kufuata maelekezo.

Kwa waombaji kwenye Vyuo visivyo vya Serikali watatakiwa kuomba moja kwa moja kwenye vyuo husika. Hivyo vyuo vya Ualimu visivyo vya Serikali vitapokea maombi na kufanya uchaguzi wa wanafunzi wenye sifa na kisha kuwasilisha NACTE majina ya waliochaguliwa kwa ajili ya uhakiki kabla ya kuyatangaza. Vyuo vinaelekezwa kuzingatia utaratibu wa udahili kwa mwaka wa masomo 2018/19.

Imetolewa na

Ofisi ya Katibu Mtendaji

Baraza la Taifa la Elimu ya Ufundi