9th September 2018 12:57:55

TAARIFA KWA VYOMBO VYA HABARI KUHUSU UKIUKWAJI WA TARATIBU ZA UDAHILI WA WANAFUNZI KATIKA KOZI MBALIMBALI ZA NGAZI YA ASTASHAHADA NA STASHAHADA KWA MUHULA WA UDAHILI WA SEPTEMBA 2018

 

TAARIFA KWA VYOMBO VYA HABARI

KUHUSU UKIUKWAJI WA TARATIBU ZA UDAHILI WA WANAFUNZI KATIKA KOZI MBALIMBALI ZA NGAZI YA ASTASHAHADA NA STASHAHADA KWA MUHULA WA UDAHILI WA SEPTEMBA 2018

Baraza la Taifa la Elimu ya Ufundi (NACTE), ni chombo kilichoanzishwa kwa mujibu wa sheria, Sura ya 129. Kwa mujibu wa sheria hiyo, Baraza linao wajibu wa kusimamia na kuhakikisha kuwa Elimu na Mafunzo ya Ufundi yanayotolewa nchini yanakidhi vigezo na ubora unaohitajika katika soko la ajira ndani na nje ya Tanzania.

Katika muktadha huo, Baraza linao wajibu wa kuhakikisha kwamba wanafunzi wanaodahiliwa katika kozi zinazosimamiwa na Baraza, wanazo sifa kwa vigezo vinavyotakiwa. Lakini pia Baraza linao wajibu wa kuwahakikishia wanafunzi na umma kwa ujumla kwamba waombaji wa kozi mbali mbali wanadahiliwa katika kozi na vyuo vinavyotambuliwa na Baraza.

Hivyo, Baraza linao wajibu wa kuhakiksha kwamba taratibu zilizowekwa kwa mujibu wa sheria zinazingatiwa na kufuatwa kwa masilahi mapana ya umma na taifa kwa ujumla.

Baraza limebaini kwa masikitiko makubwa kwamba baadhi ya Taasisi na Vyuo vinavyotoa mafunzo katika ngazi ya Cheti na Diploma 

vinakiuka taratibu zilizowekwa kwa mujibu wa sheria. Taasisi na Vyuo hivyo vimeamua kwa makusudi kutangazia umma kwamba tayari vimeanza kutoa mafunzo na kwamba wanafunzi wamechelewa hivyo wanahimizwa kufanya malipo haraka. Baadhi ya Taasisi na Vyuo hivyo pia vimekuwa vinawapelekea wanafunzi ujumbe kwa njia ya simu kwamba "hongera kwa kuchaguliwa kujiunga na chuo, na kwa utaratibu zaidi wasiliana na chuo chetu". Huku ni kuwarubuni wananchi na kuwanyima fursa za kufanya maamuzi yao kuhusiana na matakwa yao. Jambo hili lipo kinyume na taratibu.

Baraza linapenda kuufahamisha umma kwamba, masomo bado hayajaanza na kwamba baada ya mwanafunzi kuwasilisha maombi ya kujiunga na chuo katika chuo husika, mwanafunzi huyo hatasajiliwa chuoni hapo kabla ya jina lake kuhakikiwa na kupitishwa na NACTE. Majina ya wanafunzi walioomba kujiunga na vyuo mbalimbali yatawasilishwa NACTE kwa ajili ya uhakiki kuanzia tarehe 15 hadi 22 Septemba, 2018. Baada ya uhakiki huo ndipo masomo yataanza rasmi tarehe 15 Octoba, 2018.

Vyuo vilivyopata idhini ya kuanza mafunzo mapema ni:

Chuo cha Serikali za Mitaa - HomboloChuo cha Wanyama Pori - PansiasiChuo cha Mipango na Maendeleo ya Jamii (IRDP)Wakala wa Maendeleo ya Uongozi wa Elimu (ADEM) na Chuo cha Sayansi na Teknolojia Karume.